kiswahili

About GAAD

Third Thursday of Each May is Global Accessibility Awareness Day.

Select a different language to learn about Global Accessibility Awareness Day:

Kiswahili

Kila mwaka, Alhamisi ya tatu ya mwezi wa Mei, tunakualika kushiriki katika Siku ya Kuhamasisha Ufikiaji Ulimwenguni (Global Accessibility Awareness Day [GAAD]). Madhumuni ya siku hii ni kuwafanya watu wazungumze, wafikirie na wajifunze kuhusu ufikiaji wa kidijitali (tovuti, programu, simu, nk.) na ujumuishaji wa zaidi ya watu bilioni 1.2 wenye ulemavu wa aina mbalimbali kote ulimwenguni. Walengwa wa GAAD ni jamii za watu wanaojihusisha na kubuni, kukuza na kuwezesha matumizi ya teknolojia pamoja na jamii zingine husika za watu wanaounda, kufadhili na, kushawishi teknolojia na matumizi yake. Licha ya kwamba watu wanaweza kupendezwa na mada ya kufanya teknolojia ipatikane na itumike na watu wenye ulemavu, ukweli ni kwamba mara nyingi hawajui wataanzaje au wataanzia wapi. Uhamasishaji ndio hatua ya kwanza.

Soma chapisho la blogi ya Joe Devon aliloandika mnamo Novemba 2011 ambalo lilichochea juhudi hii ya ulimwengu mzima. Jennison Asuncion hakumfahamu Joe hapo awali. Lakini, kupitia Twitter, Jennison alijua kuhusu blogi hiyo punde tu baada ya kuchapishwa kwake na pamoja, wakaanzisha GAAD. GAAD iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mnamo 2012. Ili upate mawazo ya jinsi unavyoweza kushiriki katika GAAD tafadhali soma ukurasa huu (unapatikana katika lugha ya Kiingereza)  https://globalaccessibilityawarenessday.org/participate-directly

CHANGAMOTO: Ujuzi wa ufikiaji unahitaji kupewa kipaumbele na watengenezaji. SASA.

Imechapishwa na Joe Devon mnamo tarehe 27 Novemba, 2011 katika lugha ya Kiingereza https://mysqltalk.wordpress.com/2011/11/27/challenge-accessibility-know-how-needs-to-go-mainstream-with-developers-now/

Hakuna habari nyingi nzuri kuhusu ufikiaji. Itakubidi uzitafute kwa bidii. Ni wangapi kati yenu mnajua JAWS ni nini? Baada ya vidukizo vya Internet Explorer 6/7/8 na nyinginezo kujitokeza kuhakikisha kwamba kivinjari hicho kinaweza kufanya kazi na tovuti husika, je, wewe pia huangalia maudhui yako kwenye kisomaji cha skrini?

Ningependa kutoa hoja kuwa ni muhimu zaidi kufanya tovuti iweze kufikiwa kuliko kuifanya iwe ya kuvutia kwa watu wanaotumia vivinjari vya zamani. Kwa watu wengine, mtandao unaoweza kufikiwa una manufaa makubwa. Ingawa mimi ni mwandishi wa programu za kuendesha seva, bado naona aibu kwa sababu ya ufahamu wangu mdogo. Na wewe je?

Jitihada nyingi zinaelekezwa kwenye semantiki ya HTML5 kwa kusudi la ufikiaji. Nimekuwa nikitafakari wazo hili kwa miaka kadhaa, lakini sasa wakati umefika wa kuomba msaada wako. Tufanye kazi pamoja na tutatue jambo hili ambalo hatujalijumuisha katika ujuzi wetu. Kama jamii, tunaweza kufanya kazi pamoja kubadilisha ulimwengu.

Kwanza, tukubaliane kuhusu Siku ya Kuhamasisha Ufikiaji Ulimwenguni. Hii itakuwa siku ya mwaka ambapo watengenezaji wa nyavuti ulimwenguni kote watajaribu kuhamasisha umma kuhusu ufikiaji pamoja na kufunza ujuzi wa jinsi ya kufanya tovuti ziweze kufikiwa.

Siku hiyo, kila mtengenzaji wa wavuti atahimizwa kufanya majaribio kwenye angalau ukurasa mmoja wa tovuti yake akitumia zana ya ufikiaji. Baada ya kurekebisha ukurasa huo, wanahimizwa kublogi kuhusu kile walichobadilisha na kuhamasisha wengine kufuata mfano wao.

Ili kufanya mipango kwa ajili ya siku hiyo, wapangaji wa mikutano kwenye jukwaa la Meetup (www.meetup.com), kama mimi, watahimizwa kupanga kuzungumza kuhusu ufikiaji. Ikiwa unaweza kupata mtu anayetumia JAWS au kisomaji cha skrini kuhudhuria na kuelimisha, hiyo itakuwa na manufaa ya ziada. Pengine zoezi la pamoja la waandishi wa programu za kompyuta litafaa. Ikiwa wewe huzungumza kuhusu utengenezaji wa wavuti, unahimizwa kuandaa mazungumzo kuhusu mada hiyo. Wewe ni miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa katika tasnia yetu. Ikiwa mtu yeyote anayesoma habari hii anajua mashirika ambayo yangependa kushiriki katika juhudi hii, tafadhali saidia katika kuyajumuisha. Tuchague siku, sanasana tarehe 9 Mei. Siku ya Kuhamasisha Ufikiaji Ulimwenguni.

Basi unaweza kufanya nini leo? Sambaza habari. Toa mapendekezo; k.m. hashtegi nzuri ya juhudi hii inaweza kuwa gani? Ikiwa uko katika jukwaa la Meetup, anza kufanya mipango. Ikiwa hauko katika jukwaa la Meetup, jiunge nalo.